Head image
Govt. Logo

Hits 111395 |  2 online

           


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais amewaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuichangia hotuba ya bajeti, kushauri ipasavyo na hatimae waiidhinishe bajet hiyo
news phpto

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman amewaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuichangia hotuba ya bajeti, kushauri ipasavyo na hatimae waiidhinishe bajeti hiyo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman amewaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuichangia hotuba ya bajeti, kushauri ipasavyo na hatimae waiidhinishie Ofisi hio jumla ya shilingi 19,757,791,943 ili kutekeleza kazi za kawaida na kazi za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Ameyasema hayo wakati akiwasilisha utekelezaji wa mpango na bajeti kwa Taasisi zinazounda Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hio kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi, Chukwani Zanzibar.

Mhe. Harusi ameliomba Baraza la Wawakilishi kuiridhia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ichangie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali jumla ya shilingi 300,000,000 zitakazokusanywa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira.

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inashughulika na masuala mtambuka ya uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira, masuala ya Watu wenye Ulemavu, masuala ya VVU na UKIMWI na masuala yanayohusu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, pamoja na kusimamia na kuratibu Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

“Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ina dhima kubwa ya kukuza ushirikiano na wadau kutoka sekta mbali mbali kutokana na kwamba maeneo yake ya kiutendaji inayoyasimamia ni mtambuka”

Akielezea vipaumbele vya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Harusi amesema ni kushughulikia athari za kimazingira ziliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambapo miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni kuweka miundombinu ya kuzuia maji ya bahari kuingia katika maeneo ya kilimo na makaazi ya watu.

Aidha, Mpango wa Upandaji miti (Zanzibar Green Legacy) utaendelezwa kwa kushirikisha wadau wote, kuimarisha ushughulikiaji masuala ya Watu wenye Ulemavu kwa kuwatambua waliko, ulemavu wao na hatimaye kuwasajili katika mfumo utakaoiwezesha Serikali kuweka misingi ya kuimarisha haki, fursa na huduma.

Kwa kushirikiana na wadau wengine, kuanzisha mpango wa kupunguza vyanzo vya ulemavu kama vile ajali za barabarani, maradhi yasiyoambukiza, kutekeleza Sheria mpya ya Dawa za Kulevya inayoimarisha mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ili hatimaye kuweza kuinusuru jamii.

Kuendelea kupiga vita UKIMWI kwa kuendesha programu za kukuza mwitiko wa jamii ili hatimae kuweza kuuondoa UKIMWI katika orodha ya magonjwa hatarishi, kuendelea kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira, kushajihisha jamii kuwajali, kuwahudumia na kuwaendeleza Watu wenye Ulemavu.

Pia kuimarisha vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kufanya kampeni mbali mbali katika ngazi ya jamii, na kuimarisha uratibu wa masuala yanayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kuhusu muelekeo wa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi amesema programu yote imeandaliwa kwa kuzingatia nyaraka za Kitaifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa mwaka 2021-2026 (ZADEP), Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Maagizo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Mengine ni maelekezo ya Makamu wa Kwanza wa Rais aliyoyatoa kwa nyakati tofauti katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Aidha, Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais umezingatia masuala yaliyomo katika Mpango Mkakati wake wa mwaka 2021 – 2026.

Ofisi imeshughulikia mapitio ya baadhi ya zana za kufanyia kazi ikiwemo Sheria ya Dawa za Kulevya ambayo imekamilika na Sheria ya Watu wenye Ulemavu inaendelea kukamilishwa ili iwasilishwe Barazani katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Mapitio ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu yanalenga kuweka mfumo madhubuti wa kitaasisi wa usimamizi na uhifadhi wa Watu wenye Ulemavu, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 3/2015 imefanyiwa mapitio na rasimu ya mapendekezo ya sheria hiyo inafanyiwa kazi katika Tume ya Kurekebisha Sheria.

Ofisi pia imesimamia kazi ya uandaaji wa Kanuni tano za Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambazo ni kanuni ya utekelezaji wa sheria, kanuni ya viwango vidogo, kanuni ya uajiri, kanuni ya muongozo wa zawadi na kanuni ya fomu.

Aidha Mpango Mkakati wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais umetayarishwa na kwa sasa upo katika hatua ya kukamilishwa baada ya Mshauri Elekezi kumaliza kazi yake, Mhe Harusi amewashukuru wote waliochangia kufanikisha utendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kwani michango, maelekezo na ushauri wao umesaidia sana, kuongeza kasi ya utendaji kwa kuleta mafanikio ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe Waziri



Tel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz