Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia (Rihabilitation Center) ili kuwarudisha waraibu katika hali ya kawaida.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia (Rihabilitation Center) ili kuwarudisha waraibu katika hali ya kawaida.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo alipofanya ziara katika kituo cha tiba na marekebisho ya tabia kwa watumiaji wa uraibu kilichopo Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, alipofika kujionea uendeshaji wa kituo hicho pamoja na miradi iliyopo kituoni hapo.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa waraibu waliopo kituoni hapo ni rasilimali inayotegemewa kwa ujenzi wa Taifa na Familia kwa Ujumla hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa vijana waliopo katika kituo hicho na vituo vyengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuanzisha miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuwapatia ujuzi ambao utawasaidia pindi vijana hao watakapotoka kituoni hapo na kurudi katika jamii zao.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameutaka Uongozi huo kununua mashine ya kutotolea vifaranga ili kumaliza changamoto ya upatikanaji wa kuku pamoja na kuhakikisha ng’ombe wanapatikana ili kuboresha utoaji wa huduma kwa vijana waliopo kituoni hapo jambo ambalo litawasaidia kufikia malengo ya kituo hicho.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza uongozi wa Mamlaka hiyo kwa uamuzi wao wa kupunguza gharama za miradi hatua ambayo itasaidia fedha hizo kutumika katika maeneo mengine.
Akiwasalimia waraibu waliokuwepo kituoni hapo Mhe. Hemed amewataka kuwa watiifu na nidhamu ili lengo la kuwepo kituoni hapo liweze kufikiwa na Taifa lipate Vijana watakaolitumikia kwa kuleta maendeleo.
Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar Kanal Burhani Zuberi Nasoro ameeleza kuwa kituo kilianzishwa Januari 2022 ambapo kwa sasa kina Waraibu thalathini na Nne (34) ambapo lengo kuu ni kubadilisha tabia ya waraibu hao kurudi katika mazingira ya kawaida.