SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) imepitisha sheria ya watu wenye ulemavu pamoja na kuunda mabaraza ya wilaya kwa lengo la kuhakikisha wanapata haki zao kama wanavyopata watu wengine.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) imepitisha sheria ya watu wenye ulemavu pamoja na
kuunda mabaraza ya wilaya kwa lengo la kuhakikisha wanapata haki zao kama wanavyopata
watu wengine.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman ameyasema hayo
mara baada ya kumaliza kwa ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. Amesema sheria
hiyo imeshakamilika na ipo tayari kutumika ambayo itapita katika sekta zote na kusaidia kutatua
changamoto ambazo zinawakabili watu wenye ulemavu pamoja na kupatiwa haki na fursa zote.
“Sheria ya watu wenye ulemavu tayari imeshapitishwa na itakuja katika sekta zote, pamoja na
kuanzishwa kwa mabaraza ya Wilaya, ombi langu kwenu naomba tushirikiane kwa pamoja
katika kusaidia kutatua changamoto wanazozipata pamoja na kuwapatia fursa muhimu kwao”.
Waziri Harusi ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu ambapo
amesema kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za msingi pamoja na kuwadhalilisha. Aidha
Waziri huyo amesema ofisi yake ipo katika mpango wa kuhakikisha wananchi wanarudisha hali
ya mazingira ya kijani katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Amesema wameamua kufanya hivyo kutokana na kuona kijani inapotea katika visiwa hivi
ambapo bila ya kufanya hivyo madhara mengi yanaweza kupatikana. “Tusipoweka mpango
maalum wa kuirudisha kijani katika nchi yetu madhara na matatizo mengi yanaweza kutufikia,
tukifanya hivyo tunaweza kujijenga na kuimarisha ardhi pamoja na kuepukana na majanga ya
aina mdali mbali”.
Hivyo, Waziri Harusi amewataka wamiliki wa hoteli mbali mbali visiwani humu kuiga mfano
wa hoteli ya Zuri ambayo imejikita katika kulinda na kuhifadhi mazingira. Amesema wananchi
waridhie kutunza mazingira na kutunza miti na kuhakikisha haiba ya mji inaonekana.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud amesema katika Mkoa
wake tatizo la dawa za kulevya limepungua kwa kiasi kikubwa. Amesema wanachokifanya hivi
sasa ni kufuatilia kwa karibu katika hoteli na nyumba za kulala wageni kwa lengo la kuhakikisha
usambazaji na uuzwaji wa biashara hiyo haramu unaondoka katika Mkoa huo. “Serikali ya Mkoa
inawashukuru sana masheha kwa juhudi wanazozichukua katika kuhakikisha inavunja magenge
ambayo yanasabisha kuwepo kwa biashara hiyo, lakini tumeanzisha ulinzi shirikishi katika
kuondoa hilo tatizo”.
Nae muelimishaji rika kituo cha huduma rafiki Nungwi, Khamis Ali Makame amesema
kuanzishwa kwa kituo hicho kimesaidia vijana wa eneo hilo na maeneo mengine kwenda
kujifunza maswala mbali mbali. Ameeleza kwamba kuwepo kwa kituo hicho cha huduma rafiki
vijana wengi wamefanikiwa kupata elimu ambayo inawasaidia kujitambua katika maisha yao ya
kila siku. Amefahamisha kwamba vijana wengi wanaofika katika kituo hicho ni wanafunzi wa
skuli na vijana wa mitaani ambapo kwa siku wanafika zaid ya 30 katika kupata elimu ya mambo
mbali mbali.
Katika ziara hiyo Waziri Harusi alitembelea maeneo mbali mbali ikiwemo kituo cha huduma
rafiki, soko na maeneo mazingira ya bahari Nungwi, kikundi cha watu wenye ulemavu
Fukuchani na hoteli ya Zuri iliyopo Kendwa.