Head image
Govt. Logo

Hits 120684 |  2 online

           


DKT SHAJAK ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WAMIRADI YA MAENDELEO.
news phpto

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar Dkt Omar D. Shajak akiwa ndani ya uwa wa kiwanda cha sabuni kukaguwa ujenzi unaoendelea Matemwe ameongozana na mratibu wa mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kurudisha uoto wa asili Alawi Haji Hija pamoja na bi Siti Liuku Khamis ambae ni mjumbe wa Sheha wa Shehia ya Kijijini Matemwe.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar Dkt Omar D. Shajak, amesema ameridhishwa na hatua iliyofikia ya Miradi ya maendeleo ya kusaidia kuhimili mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na Idara ya Mazingira ambayo ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Matemwe kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na kuridhishwa na kazi nzuri iliyofikiwa ya utekelezaji wa maendeleo ya miradi hio pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na kuona kazi iliyobakia.

Dkt Shajak amefahamisha kuwa lengo la mradi ni kusaidia kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kwa kurejesha uoto wa asili, ambapo njia zinazotumika ni kutoa elimu juu ya kilimo chenye kustahamili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwajengea uwezo wanajamii juu ya njia mbadala za kujipatia kipato ambacho hakiathiri mazingira

Akitoa ufafanuzi juu ya njia mbadala wanazopatiwa ni kuwa tayari kumeshachimbwa visima kuweka miundombinu ya uhakika na wananchi wameanza kutumia na hivyo kwa sasa wanaweza kulima kilimo chenye tija ikiwemo cha umwagiliaji maji na baada ya kipindi kifupi faida yake itaonekana.

"Kama tulivoona ardhi yao Matemwe inarutuba ya kutosha licha ya kuwa ni ya jiwe hivyo kwa vile tushachimba visima na sasa kilichobaki shughuli kiuchumi na kijamii ziendelee”

Mbali na kuchimba visima 6 na kujenga minara ambapo kila shehia vipo visima viwili lakini mradi umejikita kwenye masuala ya uvuvi, kilimo, ushoni, ufugaji na ujasiriamali ambapo waandishi walishuhudia kiwanda cha ushoni na kiwanda cha sabuni vikiwa katika hatua ya mwisho kumalizika pamoja na boti zinazotumika kwa shughuli za uvuvi.

Ametoa rai kwa wenye hoteli za kitalii zilizoko Matemwe kuwa tayari kununua sabuni zinazotengenezwa na kiwanda cha sabuni cha Matemwe badala ya kuagiza kwengine kutokana na ubora wenye kiwango cha uzalishaji wa sabuni hizo.

Aidha Dkt.Shajak amesema wapo vijana waliopatiwa boti bure bila ya gharama yoyote ambapo amefurahishwa kuona wanazitumia vyema boti hizo, huku baadhi yao wakiwa wamejiongeza kwa kununua boti nyengine baada ya kupata faida iliyotokana na boti walizokuwa wamepewa kupitia mradi huo.

“Jambo la kujivunia mradi umezalisha ajira hivyo na niwaambie wanufaika wa mradi huu tukionesha mafanikio maendeleo ya mradi yataonekana na hivyo kuzipa nguvu Serikali zetu kuona ipo haja sasa kuendeleza miradi mengine zaidi “

Nae mratibu wa mradi huo Alawi Haji Hija alisema kuwa hatua kubwa imeshafikiwa na kazi iliyobakia ni utoaji wa mafunzo ya ufugaji na ushoni pamoja na kukamilisha majengo yote ambayo yatatumika kwa kazi hizo

Kwa upande wa mafunzo ameongeza kuwa mafunzo yamelenga zaidi katika kilimo chenye kustahamili ukame na baadae wanajamii watapatiwa nyenzo zote ambazo zitatumika katika kilimo, sambamba na kuwa wanatarajia kurejesha uoto wa asili ambapo zaidi ya heka 200 zitatumika katika kupanda miti ya aina mbali mbali.

Aliongeza kuwa katika masuala ya ufugaji wanatarajia kununua ngo'mbe ili kuwapa wananchi hao kwa ajili ya kuongeza uzalishaji mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika Febuari 2024, tokea ulivyoanzishwa mwaka 2018.

Nae sheha wa shehia ya Kijini Matemwe Msiyakwe Makame Haji alisema kwa kushirikiana na masheha wenziwe na wananchi wake watahakikisha wanasimamia vyema miradi hiyo na kuhakikisha vijana walio wengi wanaweza kujiajiri wenyewe.

Mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kurudisha uoto wa asili unatekelezwa kwenye Mkoa wa Kaskazini Unguja ndani ya Wilaya ya Kaskazini “A” Kijiji cha Matemwe katika Shehia za Matemwe Kijini, Mbuyutende, na Jukakuu Wadi wa Kijini na unasimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar

Katika mradi huo zaidi ya shilingi bilioni 1.1 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwake.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe WaziriTel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz