Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Mheshimiwa Harusi Said Suleiman akiwa katika ziara ya kimazingira na kukagua Maeneo yaliyoathiriwa na uchimbaji wa Mashimo Hatarishi ya chini kwa chini (Tunnel) Pembezoni mwa ukanda wa Bahari katika Kijiji cha Mtende,Mkoa wa Kusini Unguja:tarehe 21.02.2024.
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Mhe. Harusi Said Suleiman amewataka Wananchi na Wawekezaji kulinda Mazingira ili uwekezaji wao uwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mhe. Harusi ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi mbali mbali ya Uwekezaji na kuona jinsi inavyohifadhi mazingira.
Amesema, utunzaji wa mazingira ni muhimu na kuahidi kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaendelea kutoa elimu na hamasa ya utunzaji wa Mazingira ili Wananchi na Wageni waweze kujua umuhimu wa Mazingira Nchini.
Aidha, amemtaka Mmiliki wa mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Umbe Villas beach and Bangalore kusimamisha uchimbaji wa shimo kwa ajili ya kutengeneza njia ya ufukweni ili kujikinga na matatizo yanayoweza kujitokeza.
‘‘Huu ni uvunjifu wa Sheria na unaweza kuleta athari za kimazingira kwa jamii hivyo naomba Shimo hili lifukie mara moja.’’ Alisisitiza Waziri Harusi.