HAYATI MAGUFULI AMEACHA ALAMA TANZANIA - MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR
“Uwajibikaji ni miongoni mwa alama kubwa ambayo inanifanya nimkumbuke Hayati Magufuli,” amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, jana Jumamosi (Machi) 2021 wakati wa mazungumzo yake na kituo cha televisheni cha ITV nyumbani kwake, Osterbay jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Othman amesema Hayati Magufuli tangu akiwa naibu waziri, kisha waziri na hatimae kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alibeba sifa moja ya uwajibikaji.
”Uwajibikaji ndio sifa ya uongozi na ndicho kipimo cha utumishi wa mtu, hasa unapokuwa katika utumishi wa umma na hata taasisi binafsi, Na jambo hilo Dk. Magufuli alikuwa nalo.” alisema Mheshimiwa Othman
Makamu huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameongeza kwamba Hayati Magufuli alipenda sana kuona mambo yanafanywa na kuenda kwa haraka na ufanisi mkubwa. Akitoa mfano wa hayo, Mheshimiwa Othman amesema wapo watumishi wa umma waliokuwa wanachelewesha sana utekelezaji wa majukumu, “lakini kipindi cha awamu yake aliweza kwa kiasi kikubwa kuleta heshima hasa ya utumishi wa umma.”
Aidha, Mheshimiwa Othman amesema Hayati Magufuli alikuwa na maono ya ukombozi wa rasilimali za taifa. “Katika hili, wote ni mashahidi namna ubadhirifu uliokuwa unafanyika katika sekta ya madini na watu wachache walivyokuwa wakitumia rasilimali hizo kwa maslahi yao binafsi badala ya manufaa ya taifa.”
“Mimi sikuwa mwanasiasa hasa, bali nilikuwa mwangalizi wa siasa. Katika eneo hili, Dk. Magufuli aliweza pia kutumia nafasi yake ya kisiasa hata kuibadilisha taswira ya chama chake kwa kufichuwa ufisadi mkubwa uliokuwa ndani yake,’’ alisema Mheshimiwa Othman.
Kuhusiana na Tanzania ya baada ya Hayati Magufuli, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amempongeza Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuchukuwa rasmi nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akisema kuwa ana imani sana na utendaji wake, kwani ni kiongozi ambaye tayari ana uzoefu wa uongozi kupitia ngazi mbalimbali mpaka kufikia sasa.
Mheshimiwa Othman amesema, itapendeza sana kuona mashirikiano na mahusiano mema ya vyama vya siasa kwa sasa na kwamba hii ni fursa kwa waliopo kuhakikisha wanatengeneza namna za kuondoa tofauti na kuleta umoja wa Watanzania.
“Napenda kuliona taifa linaungana na kuleta mafanikio,” alisema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye tangu jana amekuwa akiungana na viongozi wengine wa serikali waliopo jijini Dar es Salaam kwenye shughuli zinazohusika na msiba wa Hayati John Magufuli.