Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais amefanya ziara ya kukitembelea Kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni Wilaya ya Kati Unguja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saada Mkuya Salum amefanya ziara ya kukitembelea na kukikagua Kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni Wilaya ya Kati Unguja
Katika ziara hio Dkt Saada amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Bi Kheriyangu Mgeni Khamis kufanya jitihada za makusudi na kukamilisha taratibu zilizobakia ili kituo hicho kianze kutumika kama kilivyokusudiwa
Amesema kwa vile hatua za awali zimekamilika ikiwemo uwepo wa wataalamu, kuingizwa kwa samani na vifaa mbalimbali, kuwepo kwa miundombinu na mahitaji ya umeme na maji ni vyema kujiandaa na kuhamia ili shughuli za kituo hicho zianze mara moja .
‘ kutoanza kazi kwa kituo hicho hadi sasa kutapelekea baadhi vifaa kuharibika jambo ambalo litapelekea hasara kinyume na matarajio ya Serikali’ alisisitiza Dkt Saada .
Aidha Dkt Saada amesema dira ya Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na lengo kuu inaelekeza kuwa na jamii isiyotumia dawa za kulevya hivyo kupitia Ofisi yake watahakikisha walengwa wa kituo hicho wanapatiwa kile wanachostahiki kupatiwa ili waendane na kasi ya maendeleo kufikia uchumi wa buluu
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Bi Kheriyangu Mgeni ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha vijana wanapewa malezi bora na wale ambao kwa njia moja ama nyengine wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya wanapatiwa tiba na elimu ya kuepukana na tabia hatarishi
Bi Kheriyangu amesema utekelezaji wa Tume kupitia programu kuu ni udhibiti wa Dawa za Kulevya wenye lengo la kudhibiti usafirishaji na usambazaji pamoja na kupunguza mahitaji ya matumizi ya Dawa za Kulevya
Aidha amesema majukumu ya Tume hio ni kuendeleza jitihada za kuzuia matumizi ya Dawa za Kulevya ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa hizo jambo ambalo wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa na uwepo wa kituo hicho kutawezesha kuendelea kutoa tiba na marekebisho ya tabia
‘ Ni jambo la faraja kwani kuongezeka kwa vijana waliochana na matumizi ya dawa za kulevya kumepelekea kukua na kuimarika kwa mtandao wa watu waliopata nafauu pia kufanya kazi kwa karibu na wanajamii, Taasisi za ndani zikiwemo Mamlaka ya Dawa za Kulevya Tanzania Bara, Jeshi la Polisi, Vikosi Maalum vya SMZ, Shehia nk ’
Bi Kheriyengu amewaomba wazazi na walezi wakubaliane na serikali kuwapa nafasi tena vijana walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za Kulevya warudi na wawapokee kwani tayari wamejirekebisha makosa yao na wanahitaji faraja yao
Kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni kinatarajiwa kuwa ni kitovu cha malezi ya vijana walioathirika na matumizi ya Dawa za Kulevya sehemu ambayo watapatiwa tiba sahihi na stadi za maisha, kujifunza masuala mbali bali yenye manufaa ili waendane na harakati za maendeleo kama mipango ya Serikali ilivyobainisha
Hadi sasa ujenzi wa kituo hicho umeshagharimu zaidi ya shilingi Bilioni mbili na hadi kukamilika kwake kitagharimu zaidi ya Bilioni nne za Kitanzania ambapo kilitarajiwa kuwa kimeshahamiwa lakini kutokana na ugonjwa wa Korona ilipelekea kuwekwa wagonjwa kwa muda.