Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais amesema Ofisi yake itasimamia vyema majukumu yake ili kuhakikisha masuala yote mtambuka yanakuwa salama na hayaathiriwi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt we Mkuya Salum amesema Ofisi yake itasimamia vyema majukumu yake ili kuhakikisha masuala yote mtambuka yanakuwa salama na hayaathiriwi
Ameeleza hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa programu za ofisi yake kwa kipindi cha miezi mitatu Januari na Machi 2021aliyoiwasilisha kwa Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Dkt Saada amesema Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais moja kati ya malengo yake ni kuhakikisha inakuwa na mfumo bora wa kisera na kisheria kwa taasisi inazozisimamia
Aidha amesema Kupitwa na muda kwa baadhi ya Sera na Sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ni changamoto ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi, kufanyiwa mapitio na kutoa mapendekezo ya kurekebisha Sera na Sheria hizo kwa ajili ya utekelezaji ili kuendana na kasi ya kiutendaji kwa mujibu wa taratibu
‘Rasimu ya Sera ya Dawa za Kulevya imeandaliwa na ipo katika hatua ya kuwasilishwa Baraza la Mapinduzi. Rasimu ya Sera ya Mazingira ipo katika hatua ya maandalizi na rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ipo katika hatua ya kupelekwa kwa wadau’alifafanua Dkt Saada
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Mhe Hassan Khamis Hafidh ameiomba Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhakikisha wanasimamia vyema majukumu yao ili Zanzibar iendelee kuwa salama kwa masuala wanayoyaratibu
Hassan amesema Zanzibar inahitaji kuwa salama katika kulinda na kuhifadhi mazingira, kutokubali kuwa ni sehemu ya wapitishaji na wauzaji na wasambazaji dawa za kulevya, kuzingatia vyema masuala ya upatikanaji wa haki za Watu wenye Ulemavu na kuwa na jamii isiyokuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na UKIMWI
Aidha amewataka viongozi wa Ofisi hio kuhakikisha matumizi na mapato yanaendana na utekelezaji wa mpango wa bajeti .
Akitoa maelezo ya mradi wa kujenga uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa maeneo ya pwani katika eneo la Kilimani Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi Khadija Khamis Rajab amesema mafaniko makubwa yamepatikana katika mradi huo ambapo hifadhi ya fukwe imerudi ukilinganisha awali maji yalikuwa yakiingia karibu na maeneo ya makaazi.
Mradi huo ambao umefadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa kimazingira ulianza 2013 - 2018 na shughuli zilizofanyika katika kurudisha mazingira ni upandaji wa mikoko na kuweka ukuta kwa kutumia mawe kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari yasipande juu na kuathiri maeneo ya makaazi ambapo shughuli hizo zimegharimu zaidi ya dola za kimarekani laki 4 zilizosimamiwa na wahisani wenyewe
Aidha katika kuliendeleza eneo mradi ulipewa Jumuiya ya kuhifadhi na kusimamia mazingira ZACEDY na hatua kadhaa zilichukuliwa ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, viongozi wa Wilaya na Shehia ili wapate uelewa, usafishaji wa eneo, masuala ya ufatiliaji na tathmini, shughuli za upandaji miti ambapo gharama zilizotumika ni zaidi ya Milioni 11.
Katibu wa Jumuiya inayosimamia mazingira ZACEDY kupitia eneo la mradi wa kujenga uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa maeneo ya pwani katika eneo la Kilimani ndugu Jamal Khamis Juma amesema kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kurudisha eneo hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Wilaya Mjini na wanajamii
Pia ametoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Idara ya Mazingira na Mamlaka ya usimamizi wa Mazingira kwa kuaminiwa na kuliendeleza eneo hilo .
Ndugu Jamal amesema chagamoto kubwa katika eneo hilo kwa sasa ni kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii, baadhi ya watu wasiowaaminifu kuiba miti wanayootesha ikiwemo mikoko na mivinje na kuiomba Kamati kuweza kusaidia kupata wafadhili ili waweze kuendeleza mradi huo ambao kwa sasa umemeliza muda wake
Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar awali ilitembelea na kukaguwa mradi wa kujenga uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa maeneo ya pwani katika eneo la Kilimani kisha kuonana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Othman Masoud Othman pamoja na kupokea na kuipitia taarifa ya utekelezaji wa programu za ofisi yake kwa kipindi cha miezi mitatu Januari na Machi 2021