Head image
Govt. Logo

Hits 98050 |  5 online

           


Dkt Saada amesema mwelekeo wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Taasisi zake ni kuwa sehemu ya ujenzi wa uchumi imara,
news phpto

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kufikia Dira iliyojiwekea imedhamiria kuimarisha uwajibikaji kwa watendaji na kufanya mapitio ya miundo ya baadhi ya Taasisi zake, kuwashirikisha na kuwaweka karibu wadau kwa karibu zaidi

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kufikia Dira iliyojiwekea imedhamiria kuimarisha uwajibikaji kwa watendaji na kufanya mapitio ya miundo ya baadhi ya Taasisi zake, kuwashirikisha na kuwaweka karibu wadau kwa karibu zaidi.

Ili kufikia malengo hayo Ofisi imejipanga kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo utoaji wa taaluma na ushajihishaji wa wananchi kwa kutumia mbinu za kisasa zaidi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Saada Mkuya Salum ameyasema hayo wakati akiwasilisha Hotuba ya bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021 -2022 kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.

Dkt Saada amesema mwelekeo wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Taasisi zake ni kuwa sehemu ya ujenzi wa uchumi imara, salama na shirikishi, kwa kuimarisha mifumo kuwa bora zaidi, madhubuti na endelevu ya kusimamia masuala mtambuka ya Watu wenye Ulemavu, Mazingira, VVU na UKIMWI pamoja na udhibiti wa Dawa za Kulevya.

Muono wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ni kwenda sambamba na sera na mikakati iliyowekwa na Serikali ya kufikia malengo ya uchumi na kuhakikisha kuwa wananchi wa makundi yote wanawezeshwa na kuwa sehemu ya ujenzi wa uchumi huo.

Aidha amesema Ofisi yake inakusudia kuratibu na kufanya tafiti tatu zinazohusiana na masuala ya Watu wenye Ulemavu na UKIMWI pamoja na kuzipitia sera na sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ili ziendane na wakati wa sasa.

Kwa kutambua kuwa asilimia kubwa ya wajenzi wa uchumi wa Zanzibar ni vijana ambao wamo kwenye hatari ya kuathiriwa na matumizi ya madawa ya kulevya Ofisi itaendelea kuwasaidia kutojiingiza katika dimbwi hilo na kuwakinga wasiambukizwe Virusi vya UKIMWI.

Kwa upande wa Idara ya Mazingira na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Dkr Saada amelihakikishia Baraza la Wawakilishi kuwa Ofisi itahakikisha kuwa tathmini za athari za kimazingira na kijamii, zinafanywa kwa miradi yote ya kimaendeleo na kiuchumi,Ili kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu, ufatiliaji wa kimazingira kwa maeneo ya miradi ya kiuchumi na kimaendeleo Unguja na Pemba itaendelea ili kuhakikisha uharibifu na uchafuzi wa mazingira unapungua kwa kutoa miongozo mbali mbali.

Akielezea vipaumbele vya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkr Saada ametaja kuwa ni pamoja na kufanya tafiti ambazo zitasaidia mipango ya maendeleo ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu ya masuala mtambuka, pamoja na usimamizi na uhifadhi madhubuti wa mazingira kwa maendeleo endelevu hapa Zanzibar.

Upatikanaji na usimamizi wa haki na fursa sawa kwa Watu Wenye Ulemavu katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi, Udhibiti madhubuti wa uingizaji, usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambao utaambatana na mikakati ya kuwapatia matibabu waathirika.

Kuendelea kuimarisha mazingira ya utendaji kazi pamoja na kutoa stahiki za watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ueledi na ufanisi.

Aidha, Dkt Saada ameahidi kuendeleza mashirikiano na Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na nchi nyingine katika kuratibu masuala ya kikanda na kimataifa yanayohusu Mazingira, UKIMWI, Dawa za Kulevya na Watu Wenye Ulemavu.

Dkt Saada amevishukuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa elimu na kutangaza matukio mbali mbali yanayohusu shughuli za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Pamoja na wahusika wote walioshirikiana na ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.

Akisoma hotuba ya maoni ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kuhusu makadirio na mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mwenyekiti wa Kamati hio Mhe Hassan Khamis Hafidh amezishauri taasisi za Serikali zenye mnasaba na utunzaji wa mazingira zishirikiane katika kutunza uasili wa nchi yetu ili kizazi kijacho kiweze kunufaika na mazingira mazuri.

Mhe Hassan amesema kuwa Kamati yake imebaini kuwa ujenzi holela usiofuata sheria na taratibu pamoja na huduma za kijamii ambazo zinaondoa haiba na muonekano wa mazingira na uoto wa asili kama shughuli za uchimbaji holela wa mchanga, mawe, fusi na hasa katika miradi mikubwa ya Serikali ambayo huacha mashimo makubwa bila kufukiwa.

Kamati pia imeishauri Serikali katika Sensa ya Taifa inayotarajiwa kufanyika mwaka wa fedha 2021-2022 kuwe na kipengele maalum kwa ajili ya kukusanya taarifa za Watu wenye Ulemavu wenye mahitaji maalum ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuimarisha mfumo wa kielektroniki.

Kamati hio imebaini matumizi ya dawa za kulevya na mapenzi ya jinsia moja ni chachu ya ongezeko la maambukizi ya VIRUSI vya UKIMWI na kushauri Tume ya Ukimwi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii ili kuongeza kasi ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha kwa upande wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kamati imeshauri kuwepo mashirikiano mazuri na yenye tija kati ya Tume na vyombo vya usimamizi na utoaji wa haki ikiwemo Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mahakama ili kutokomeza kabisa biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Ili Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais iweze kutekeleza kazi zake imeliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya shilingi 12,332,922,600 kwa kazi za kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe WaziriTel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz