Head image
Govt. Logo

Hits 120658 |  3 online

           


Shughuli za kiwanda cha kusaga kokoto zasitishwa kwa muda.
news phpto

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amesitisha kwa muda shughuli za kusaga kokoto katika viwanda vya matofali hadi pale serikali itakapotoa muongozo maalum juu ya uendeshaji wa shughuli hizo.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amesitisha kwa muda shughuli za kusaga kokoto katika viwanda vya matofali hadi pale serikali itakapotoa muongozo maalum juu ya uendeshaji wa shughuli hizo.

Dk. Mkuya alieleza hayo kwa nyakati tofauti maeneo ya Bumbwini na Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, alipokuwa katika ziara ya kukagua maeneo hayo na kuona athari wanazozipata wananchi.

Alisema ili kuhakikisha usalama wa mazingira na wananchi, muongozo utatolewa kuonesha utaratibu wa kufanya shughuli hizo bila ya kuathiri mazingira

Alifahamisha kwamba uwepo wa viwanda hivyo karibu na makaazi ya wananchi kunasababisha madhara mbali mbali yakiwemo ya uharibifu wa mazingira, afya na hata vipando vyao.

Aidha Dkt Saada amesema licha ya Serikali kuwasisitiza wananchi kuwekeza katika shughuli za kiuchumi, hawapaswi kuachiwa kuleta athari ambazo zitavuruga mfumo mzima wa maisha yao.

“Serikali inawataka wawekezaji wawekeze katika sekta tofauti kwa kuamini kwamba kufanya hivyo ni mwarubaini wa kutatua changamoto hususani za ajira kwa vijana, kuongeza mapato ya mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla,” alieleza Dk. Saada.

Sambamba na hayo alisema zoezi hilo litakuwa endelevu kwa kuangalia viwanda vyote vinavyofanya shughuli hizo ili kuvifanya viwanda hivyo kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kuondosha malalamiko.

Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wanapobaini hitilafu yoyote juu ya uharibifu wa mazingira kwa namna moja au nyengine ni vyema kuripoti sehemu husika ili Serikali iweze kufatilia na kuchukua hatua za haraka kabla hakujatokezea athari zaidi .

Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakitoa huduma muhimu kwa jamii ikiwemo kuchimba visima kwa ajili ya kupatikana maji safi na salama pamoja na huduma nyenginezo.

Hata hivyo aliwasisitiza wawekezaji hao kutotumia mwanya huo kwa kuwakandamiza wengine kwani kila mtu anahaki ya kuishi akiwa na amani bila ya kubughudhiwa.

“Kila muwekezaji mwenye uwezo, muhimu kusaidia wananchi kwa namna moja au nyengine katika nyanja mbali mbali za kimaendeleo, kwani kufanya hivyo mnaisaidia Serikali kuweka mazingira mazuri ya maisha ya wananchi,” aliongeza Dk. Saada.

Hata hivyo aliwataka wawekezaji na wananchi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayohusiana na uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kulipa umuhimu suala la uhifadhi wa mazingira.

Aliongeza kuwa kufanya hivyo kutaongeza usalama wa afya za wananchi na kutoa fursa za ajira na kilimo mambo yatakayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Mbali ya uchumi bado tuzingatie usalama wa afya na maisha ya wananchi wetu na hili linawezekana kwa kufanya uwekezaji wa miradi na kuwa endelevu kwa kuweka kuta zitakazotenganisha maeneo ya uwekezaji na makaazi ya wananchi,” alieleza Dk. Mkuya.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Sheha Mjaja Juma, alisema ni vyema kwa viwanda vyote vya matofali hivi sasa kufuata utaratibu wa zamani wa kufanya matofali matupu kutokana na rasilimali ya mchanga hivi sasa upatikanaji wake hauna shida.

Mjaja alisema endapo wananchi hao wanataka kufanya biashara ya kusaga kokoto ni vyema mashine zao kuzihamishia maeneo ya kuchimbwa mawe kwa utaratibu maalum utakaowekwa ili kuondosha usumbufu na athari zinazojitokeza katika maeneo yanayolalamikiwa.

Nae Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Nishati na Madini, Omar Saleh Mohammed, alisema hivi sasa wapo katika kufanya marekebisho kwa baadhi ya kanuni ya mali asili zisizorejesheka hivyo suala hilo likikaa sawa wateweza kutoa maelekezo yanayostahiki katika maeneo hayo.

Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na kiwanda cha kokoto na matofali kilichopo shehia ya Mangapwani, Abdu Suleiman Juma, alisema uwepo wa kiwanda hicho kimewaathiri kiafya na kuharibika kwa vipando vyake.

Alisema katika eneo hilo yeye alilima mazao yakiwemo ya vanilla, matango na bidhaa nyengine lakini zote hakubahatika kuvuna kutokana na kuharibika na vumbi linalotoka kiwandani hapo na kusababisha kupata athari kubwa.

Kwa upande wake, Mmoja ya wamiliki wa kiwanda hicho, Soud Abdallah Nassor, alisema malalamiko hayo yapo kwa muda mrefu kutokana na Zanzibar kutotengwa maeneo maalum ya viwanda na makaazi ya wananchi.

Alieleza kuwa hali hiyo husababisha kutokezea kwa tofauti hizo na kutumia fursa hiyo kuiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa upana wake ili kila mtu aweze kunufaika na kuishi kwa amani.

Ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Saada ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwamba viongozi waende kwa wananchi kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Katika ziara hiyo Dk. Saada aliambatana na watendaji wake ikiwemo Katibu Mkuu Bi Khadija Khamis Rajab, Wakurugenzi kutoka Idara na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na maofisa wao, Mwakilishi wa Jimbo la Bumbwini Mhe Mtumwa Peya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Nishati na Madini ndugu Omar Saleh.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe WaziriTel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz