Mhe Dkt Saada Salum Mkuya amefanya ziara ya kutembelea Kambi ya Waanika madagaa iliyopo Mangapwani na kushuhudia mazingira yasiyoridhisha kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu muhimu katika kambi hio
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saada Salum Mkuya amefanya ziara ya kutembelea Kambi ya Waanika madagaa iliyopo Mangapwani na kushuhudia mazingira yasiyoridhisha kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu muhimu katika kambi hio
Dkt Saada ameahidi kukaa pamoja na wahusika wengine pamoja na kamati ya waanika madagaa ili kuondosha changamoto ya eneo hilo lenye harakati za kiuchumi zinazopelekea kuingia na kutoka kwa wenyeji na wageni
Hatua hizo ni pamoja na kupeleka wataalaamu kutoka Mazingira Tume ya UKIMWI na Tume ya Kitaifa Kuratibu na kupambana na Dawa za Kulevya ili kutoa elimu kwa usalama wa waanika madagaa na wauzaji wa jumla kwenye kambi hiyo
Dkt Saada amesema hatua nyengine ni pamoja na kuchukuliwa hatua za haraka kwa kuweka miundo mbinu ya uhakika ili kuepuka maradhi yanayoweza kutokea ikiwemo ya mripuko kama kipindupindu
Nao baadhi ya wanakambi wa eneo hilo wamelalamikia kutofanyiwa kazi malalamiko yao ya muda mrefu ikiwemo kupatiwa huduma ya maji na vyoo ambapo wameshauri fedha zinazochangishwa na Halmashauri kila mwezi kuwasaidia kuweka miundombinu ya kudumu
Katika ziara hio Dkt Saada amefuatana na Mwakilishi wa Jimbo la Bumbwini Mhe Mtumwa Peya na kukiri changamoto hio ni ya muda mrefu na tayari wameshakaa pamoja na Kamati ya waanika madagaa kwa kushirikiana na sheha wa shehia na taarifa ya changamoto hizo zimeshafikishwa kwa Mkuu wa Wilaya Kaskazini B
Zaidi ya watu 400 ya waaanika madagaa hueka kambi kwa wakati mmoja wakati wa bamvua la msimu wa madagaa ambapo wanunuzi wakubwa ni Wacongo ambao nao wamelalamikiwa bei ndogo wanayonunulia ikilinganishwa na gharama kubwa wanazotumia waanika madagaa hao
Aidha wauza madagaa hao wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka viwango maalum kwa wanunuzi wa madagaa kama inavyowekwa bei za mchele ili kumkomboa Mwananchi kiuchumi