Head image
Govt. Logo

Hits 113650 |  1 online

           


Siku ya Maadhimisho ya Kupinga Matumizi na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya Duniani.
news phpto

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika jukwaa akipokea Maandamano ya Kilele cha Siku ya Maadhimisho ya Kupinga Matumizi na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya Duniani.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika jukwaa akipokea Maandamano ya Kilele cha Siku ya Maadhimisho ya Kupinga Matumizi na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya Duniani, zilizoadhimisha Zanzibar katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati umefika wa Wazanzibari kuungana pamoja katika vita dhidi ya usafirishaji na matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na kuvitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanyakazi kwa weledi na ufanisi.Dk. Mwinyi ametoa rai hiyo leo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya kupinga matumizi na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya Duniani, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema ili kufanikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kuna umuhimu wa jamii kuungana, huku akivitaka Vyombo vya Ulinzi na Usamala pamoja na taasisi nyengine zinazohusika na mapambano hayo, ikiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama na Ofisi ya Mkemia Mkuu kufanyakazi kwa misingi ya sheria na kuondokana na kasoro mbali mbali ziliopo.

Alisema azma ya Serikali ya kuibadili Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya kuwa Mamlaka; inalenga kuwa na kikosi chenye nguvu kitakachokuwa na uwezo wa kupeleleza, kukamata na kuzifikisha mahakamani kesi zinazohusiana na makosa hayo.

Alisema wakati Wazanzibari wanaungana na mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hiyo, wanapaswa kutambua kuwa kila mmoja ni muhanga wa atahri zitokazonazo na biashara hiyo haramu; kiafya, kiuchumi na kijamii.

Alieleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya katika jamii husababisha kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, kama vile wizi na unyang’anyi, matukio ya vifo, ajali, ugonjwa wa akili na kujamiiana, ulemavu pamoja na kuongezeka kwa umasikini.

“…zaidi ya yote biashara hii inachangia sana kutokuwepo kwa hali ya amani na utulivu katika jamii”, alisema.

Rais Dk. Mwinyi alisema wakati huu wa maadhimisho wananchi wanapaswa kutafakari na kubuni mbinu, mipango na kuwa na mikakati imara itakayofaa kutumika katika mapambano hayo, huku akibainisha ukubwa wa vita hivyo vinavyojhitaji ushiriki wa kila mwananchi.

Alishauri kuwepo malezi ya pamoja katika familia ili kuwafunza vijana maadili mema pamoja na kuwaelimisha athari za dawa za kulevya, sambamba na kuwafundisha stadi za maisha ili waweze kujitambua na kujilinda.

“Vikundi vya sanaa na michezo vitumike kutoa elimu pamoja na viongozi wa Dimi na wengine wa kijamii lazima washirikiane katika kupambana na tatizo hili”, alisema.

Alisema taarifa za matumizi ya dawa za kulevya kwa njia za kujidunga sindano, zinabainisha kuwepo wastani wa watu 3,200, wakati ambapo wataalamu wanaieleza hatua hiyo kuwa ni chanzo kikuu cha kuenea kwa kasi maradhi ya UKIMWI, virusi vya Homa ya Ini, maradhi ya Moyo, Figo pamoja na tatizo la ugonjwa wa akili.

Dk. Mwinyi alisema Serikali kwa kushirikiana na taasisi za kiraia pamoja na taasisi za kimataifa zinaendelea kufanya juhudi mbali mbali

Ikiwemo ya kuelimisha wananchi juu ya athari zitokanazo na janga hilo, kutunga sheria pamoja na kutoa huduma kwa waathirika.

Alisema serikali kupitia Tume ya kuratibu na kudhibiti Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali za ndani na nje ya nchi, ipo katika hatua za mwisho ya kukamilisha Kituo cha Tiba na Marekebisho ya Tabia kiliopo Kidimni Wilaya Kati Unguja ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 60.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana waliofuzu kuondokana na matumzii ya dawa za kulevya kupitia ‘sober houses’ pamoja na wale walioanza kuchukua hatua kama hiyo.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto inaendelea kutoa dawa ya Methadone katika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo Chekundu, ambapo karibu vijana 875 wamejisajili kupatiwa huduma hizo”, alisema.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kutimizia wajibu wake katika kuviimarisha vyombo vya Dola kwa kuvipatia vifaa vya kisasa vya uchunguzi na mafunzo na kuwajengea uwezo watendaji wake, sambamba na kuimarisha ulinzi katika viwanja vya ndege, bandari rasmi na bandari bubu, ikiwa ni hatua ya kukabiliana vilivyo na janga hilo.

Nae, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya, Hemed Suleiman Abdalla alisema mapendekezo ya kuibadili Tume hiyo na kuwa Mamlaka yanalenga kuleta ufanisi na kuiwezesha Zanzibar kuondokana na janga hilo na kusema kazi hiyo itawahusisha Wazanzibari wote.

Alisema vita hiyo ni kubwa na kuna uwezekano mkubwa wa kutokea majaribio mbali mbali wakati wa utekelezaji wake, hivyo akaahidi kufanyika kwa weledi na bila kumuonea mtu.

Alisema katika utekelezaji wa kazi hiyo Serikali itahakikisha kunakuwa na watu wenye sifa zinazostahili katika vyombo vya maamuzi, ili iweze kufanyika kwa weledi na kukamilika katika kipindi kifupi.

Alitumia fursa hiyo kuwataka Wazanzibari kuanzia ngazi ya shehiya kuungana na kushiriki kikamilifu katika mapambano hayo.

Mapema, Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Sada Mkuya Salum, alisema kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza kabisa nguvu kazi ya taifa katika kipindi cha miaka 20 ijayo, kutokana na kasi ya uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini ilivyo hivi sasa.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya Kanali Burhan Nassor alisema kumekuwepo changamoto mbali mbali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hususas katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, akitoa mfano wa Jeshi la Polisi ambapo mnamo mwaka 2018/19 jumla ya kesi 20 za makosa hayo zilifungwa na washtakiwa kuachiwa huru kutokana na sababu za Mkemia Mkuu kushidnwa kufika Mahakamani.

Alisema Idara ya Mahakama nayo imekuwa ikilalamikiwa kwa mamuzi yake, huku baadhi ya kesi zikionekana kutawaliwa na mazingira ya rushwa na uzembe, ukosefu wa maadili na kukosa nia thabiti ya kuiepusha nchi na janga hilo.

Kanali Nassor Alitoa mfano wa kesi namba 100/2020 iliomuhusisha Raia wa Bulgaria aliepatikana na Dawa aina ya Heroin ambayo ilifutwa baada ya Mahakama kukosa fedha za kulipia Mkalimani wa kutafsiri lugha ya Kirusi ambapo gharama yake ilikuwa Dola 200, wakati dawa alizokamatwa nazo zilikuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 100.

Alifafanua kuwa mbali na Kifungu namba 25 cha sheria namba 9 ya 2009 ya udhibiri wa Dawa za Kulevya kuzuia dhamana kwa wahalifu wa makosa hayo wanaokamtwa na viwango vikubwa, lakini wahalifu ikiwemo wageni wamekuwa wakipewa dhamana, sambamba na kifungu cha sheria namba 9 ya 2019 cha kutaifisha mali, kuachwa kutumika katika adhabu za mahakama.

Aidha, salamu za wana Jumuiya ya vijana waliopata nafuu kutokana na matumizii ya Dawa za Kulevya, ilibainisha miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana hao baada ya kutoka ‘Sobber houses’ ni kwa waathirika kurejea katika matumizi ya dawa hizo baada ya kukosa shughuli maalum za kufanya, pamoja na kuiomba jamii kuendeleea kuwasaidia waathirika badala ya kuwanyanyapaa.

Katika hafla hiyo Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki katika maadhimisho hayo, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said , Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe Waziri



Tel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz