Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuna haja ya kutilia mkazo elimu ya mazingira, ili kuinusuru Nchi kutokana na majanga ya athari mbaya za mabadiliko ya tabia nchi.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuna haja ya kutilia mkazo elimu ya mazingira, ili kuinusuru Nchi kutokana na majanga ya athari mbaya za mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo ndani ya Ukumbi wa Jumba la Makumbusho ya Wananchi Forodhani mjini Unguja, katika Kikao Maalum cha Tathmini ya Ziara yake ya kimazingira ya hivi karibuni, alipotembelea maeneo mbali mbali ya Mikoa mitatu ya kisiwa cha Unguja.
Amesema pamoja na mikakati inayoambatana na mbinu mbadala za kitaalamu sambamba na juhudi za upandaji miti kama hatua za msingi, bali suala la elimu ya mazingira lina umuhimu wa pekee katika kujenga utamaduni wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Othman amesema licha ya ukweli kwamba Zanzibar kama ilivyo kwa nchi za ukanda wote wa pwani, iko hatarini kukabiliwa na athari za kimazingira, kunahitajika mipango madhubuti ambayo ni pamoja na tathmini ya hali halisi ilivyo sasa ili kukabiliana na athari hizo.
Naye Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Masoud Ali Mohamed amefahamisha haja ya kuwepo chombo maalum cha kudhibiti na kuratibu raslimali muhimu zinazopelekea uharibifu wa mazingira ambazo ni pamoja uchimbaji wa mchanga, mawe, kifusi, misitu na matumizi sahihi ya fukwe za bahari.
Kikao hicho kimewajumuisha mawaziri, viongozi na watendaji mbali mbali wa Serikali, ambao ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Saada Mkuya Salum, Wakuu wa Mikoa, Mkoa ya Mjini Magharibi, Kaskazini na Kusini Unguja, Bw. Idris Kitwana Mustafa, Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud, na Bw. Rashid Hadid, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Omar DadiĀ Shajak, na Wakuu wa Wilaya za Unguja, Katibu Tawala na baadhi ya Wadau wa Mazingira.