Head image
Govt. Logo

Hits 98026 |  3 online

           


Dk.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa Saini ya Makubaliano ya kupambana na Dawa za kulevya na Uhalifu Zanzibar
news phpto

Dk.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa Saini ya Makubaliano ya kupambana na Dawa za kulevya na Uhalifu Zanzibar iliyotiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Kanal Burhani Zuberi Nassor akitia saini kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Afisa Muandamizi wa Ubalozi wa Uingereza Nchi Tanzania anayeshughulikia masuala ya Haki na Usalama Bw. Saimon Charters,akisaini kwa niaba ya Serikali ya Uingereza hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa misaada mbali mbali inayoipatia Zanzibar.Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipozungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David Concar.Amesema hatua ya Serikali ya Uingereza ya kusaini Hati ya makubaliano (MoU) kati yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwa ni miongoni mwa hatua muhimu katika kukabiliana na uhalifu.

Alieleza kwa vile Zanzibar ni kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki,kuna umuhimu mkubwa wakuhakikisha suala la kupambana na uhalifu linapewa nafasi, hivyo akatumia fursa hiyo kuiomba Uingereza kusaidia vifaa vya uchunguzi (body scanner) katika viwanja vyake vya Ndege na Bandarini.Aidha, alimweleza Balozi huyo kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na hali ya uhalifu ilivyo hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi alimhakikishia Balozi Concar kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kutoa udhamini kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi mbalimbali, sambamba na kupongeza azma ya kufanyika kwa Jukwaa la kibiashara kati ya Uingereza na Zanzibar, baadae mwakani na kusema hatua hiyo itaitangaza Zanzibar Kimataifa.

Aidha, alisema suala la udhibiti wa uhalifu katika eneo la bahari linahitaji Teknolojia mbali mbali, hivyo akaiomba Uingereza kusaidia katika nyanja hiyo ili kukimarisha Kikosi cha kuuzuia magendo (KMKM).Alisema pamoja na kuwepo janga la ugonjwa wa Covid – 19 Duniani, kumekuwepo na ongezeko la idadi ya Watalii wanaoingia Zanzibar mwaka huu, hususan kutoka Mataifa ya Ulaya Mashariki.

Nae, Balozi David Concar alieleza kufurahishwa na utayari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaini Hati hiyo ya makubaliano huo na kusema mashirikiano ndio njia pekee ya kukabiliana na uhalifu.Alisema Kihistoria Zanzibar ni kitovu cha Biashara, hatua inayoifanya muda wote kuwa katika shabaha ya wahalifu.

Balozi Concar alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi na kusisitiza azma ya kufanya kazi nae kwa karibu, huku akitumia fursa hiyo kumpongeza kwa mafanikio yalioanza kupatikana.Alisema Serikali ya Uingereza itafanya juhudi kusaidia upatikanaji wa taasisi zinazotoa mikopo nafuu ili iweze kuimarisha miundo mbinu ya barabara pamoja na Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba.

Wakati huo huo, akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Sada Mkuya Salum alisema Hati ya Makubaliano (MOU) iliotiwa saini kati ya Serikali ya Uingereza na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaiwezesha Uingereza kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbali mbali za kukabiliana na uhalifu, hususan wa dawa za kulevya.

Alisema wiki ijayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kubadili sheria kutoka Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya na kuwa Mamlaka ili kuiwezesha kuwa na nguvu za kisheria katika kupambana na uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya.Aidha, alisema Serikali ya Uingereza itasaidia katika kuwajengea uwezo watendaji wa Mamlaka hiyo katika maeneo tofauti ili waweze kusimamia vyema utekelezaji wa sheria, sambamba na kusaidia upatikanaji wa vifaa.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kupamba na dawa za Kulevya Kanali Burhan Nassor alisema lengo la kutia saini MOU ni kuijengea uwezo Tume hiyo ili iweze kupambana kikamilifu na wahalifu wa dawa za kulevya.Alisema kuna wahisani mbali mbali wanaosaidia mapambano hayo, ikiwemo UNODC ambayo imenoyesha nia ya kuleta vifaa vya uchunguzi (body screen mashine) kwa ajili ya matumizi katika milango yote ya kuingilia nchini.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kuachana na biashara hiyo kwani hivi sasa wataweza kushikwa kupitia teknolojia ya kisasa.

Katika hafla hiyo, Ofisa mwandamizi wa Ubalozi wa Uingerza nchini Tanzania anaeshughulikia masuala ya haki na Usalama Simon Charters alitia saini kwa upande wa Serikali ya Uingereza, wakati ambapo Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya Kanali Burhan Nassor alitia saini kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe WaziriTel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz