Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mh Dkt Saada Mkuya Salum ameishauri Kamati ya ya utekelezaji wa mkakati wa kuandaa mpango kazi wa kitaifa kutoka Taasisi ya Mwalim Nyerere kuhakikisha utafiti wanaoufanya unaigusa Zanzibar kwenye maeneo muhimu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mh Dkt Saada Mkuya Salum ameishauri Kamati ya ya utekelezaji wa mkakati wa kuandaa mpango kazi wa kitaifa kutoka Taasisi ya Mwalim Nyerere kuhakikisha utafiti wanaoufanya unaigusa Zanzibar kwenye maeneo muhimu
Dkt Saada ameyasema hayo alipokutana na baadhi ya wajumbe wa kamati hio ofisini kwake Migombani walipofika kujitambulisha na kuelezea dhamira yao yenye lengo kufanya maandalizi ya utafiti kuelekea kuandaa mpango huo unaotegemewa kuanza mwezi Januari mwaka 2022
Ameshauri kuwa ni vyema utafiti kuyagusia maeneo ya visiwa vya Unguja na Pemba kulingana na nafasi yake bila kusahau na kuangalia mila, tamaduni na mazingira yake kwa kuhakikisha tafiti hizo zinagusa masuala ya usawa wa kijinsia ukizingatia kuwa Zanzibar ina eneo dogo kulinganisha na Tanzania Bara
“Ili uweze kuziona changamoto za Zanzibar ni muhimu kuekewa eneo maalumu katika mpango kazi huo unaoandaliwa pamoja na kuweka mifano hai itakayoonesha hali halisi ilivyo kulingana na utafiti kwani tatizo la udhalilishaji ni kubwa hivyo ni vyema kufahamu kiini cha tatizo” alisisitiza Dkt Saada
Dkt Saada ambae pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar UWAWAZA ameishukuru kamati hio kwa kumuona kuwa ni mmoja kati ya mwanaharakati na kiongozi wanaoshiriki maumivu ya wanawake wanaopinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji ambapo ameahidi Ofisi yake na mwenyewe binafsi itatoa ushirikiano wa kutosha
Nae Dkt Tatu Nyange Mjumbe wa Kamati hio amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia mkataba na Taasisi ya Mwalim Nyerere ili kuandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1325 yanayohusu ajenda ya Wanawake Amani na Usalama
Amemueleza Dkt Saada kuwa makubaliano hayo yanasisitiza kuandaa mpango kazi kama ni muongozo kwa ajili ya wanawake, Amani na usalama na ifikapo Mwezi wa Januari itakuja kamati maalum ya utafiti na hivyo uwepo wao ni kuja kuandaa mazingira kufahamu kina nani watawahusisha na kufikia malengo kwa urahisi
Aidha Afisa utafiti Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Dkt Salum Ahmeid ambae ni mjumbe wa kamati hio anaeiwakilisha Zanzibar amesema tayari kamati hiyo imeshaanza kazi katika Mkoa wa Kusini Pemba na kwa Unguja itahusisha Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Tanzania Bara itahusisha mikoa 10