Waziri wa Nchi ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saada Mkuya Salum amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kutasaidia kupungua kwa kiasi kikubwa makosa yanayohusiana na utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya
Waziri wa Nchi ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saada Mkuya Salum amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kutasaidia kupungua kwa kiasi kikubwa makosa yanayohusiana na utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya
Kuanzisha Mamlaka itakayokuwa na uwezo kamili wa kukabiliana na uhalifu kutapelekea kupunguza athari zitokanazo na dawa za kulevya, kuimarika kwa nguvu kazi hasa vijana na hatimaye kukuza uchumi wa nchi
Dkt. Saada ameyasema hayo kwenye mkutano wa tano wa Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha Mswada wa Sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, kazi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inayopendekezwa itakuwa na uwezo wa kupeleleza, kukamata, kuchunguza na hatimae kupeleka Mahkamani mashauri yanayohusiana na dawa za kulevya pamoja na makosa mengine yanayofanana nayo
Dkt Saada amekumbushia dhamira njema ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kusimamia kwa vitendo ibara ya 196 (a - g) ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 -2025 kwa kuhakikisha kwamba Serikali ya Awamu ya nane inaimarisha mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya
“Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameamuwa kuibadilisha Taasisi inayoshughulikia Dawa hizo za Kulevya kutoka Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itayokuwa na uwezo kamili wa kisheria wa kukabiliana kikamilifu na uhalifu huu wa Dawa za Kulevya nchini” alisisitiza
Mapambano kwenye tasnia ya kudhibiti dawa za kulevya yanahitaji mabadiliko makubwa, ikiwemo kuifuta Sheria ya Udhibiti na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya, Nam. 9 ya mwaka 2009 inayotumika hivi sasa na kutunga Sheria mpya
Aidha Dkt Saada amesema maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ya kimtandao yanatumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya na hivyo kupelekea jitihada zilizopangwa kufanywa na mtandao wa taasisi za kudhibiti Dawa za Kulevya kuingiliwa na kuharibu ushahidi
Ukuaji wa sayansi na teknolojia unaotokea ulimwenguni kwa sasa unatoa fursa kwa wahalifu wa dawa za kulevya kuwa na mbinu thabiti za kujikinga na hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao, Ukweli huu unalazimisha kuwepo na chombo imara na thabiti cha kusimamia udhibiti wa dawa za kulevya.
Hivyo Mswada wa sheria unaopendekezwa na Serikali pia utapelekea kuongeza ufanisi katika kupambana na uhalifu wa Dawa za Kulevya nchini, ugeuzaji wa kemikali bashrifu pamoja na udhibiti wa dawa tiba.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa Mhe Hassan Khamis Hafidh katika hotuba ya maoni ya kamati hio amewaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuujadili na kuuchangia mswaada huo hatimae kuupitisha
Mhe Hassan amesema kuwa kupitishwa kwa Mswaada huo kutapelekea kupunguza changamoto zinazowakabili vijana ambao ndio nguzo pekee ya kulijenga Taifa huku akisisitiza kuwa sera na sheria zenye muundo kama huu ndio uliowasaidia mataifa mengine kufikia malengo katika kupambana na dawa za kulevya
Wakichangia Mswaada huo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameshauri kuwepo kwa udhibiti wa kina katika bandari na viwanja vya ndege na kuiomba Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhakikisha wanatunga kanuni mara tu mswaada wa sheria ya kuanzisha Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya utakapopitishwa
Mnamo mwaka 2009 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lilitunga sheria mpya No. 9 ya 2009 iliyojulikana kama Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya lakini Sheria hii imeonekana kuwa na mapungufu
Moja kati ya mapungufu ya Sheria hiyo ni kutokuwa na uwezo kamili wa kudhibiti na kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, usafirishaji, ugeuzaji wa kemikali bashirifu na udhibiti wa dawa tiba.
Mswada wa Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, uliowasilishwa umegawika katika sehemu kuu nane na kujumuisha vifungu 86 vilivyozingatia masharti mbali mbali yanayohusiana na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya
Kati ya hivyo vifungu 26 ni makatazo juu ya mambo mbali mbali yanayohusu uhalifu wa dawa za kulevya na makosa yanayo fanana nayo