Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi yaridhishwa na maendeleo ya Miradi ya Uviko 19 na miradi ya Maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman amewakumbusha wananchi kufuata sheria na kuhakikisha wanazidisha mapambano katika kulinda mazingira na kutunza vyanzo vya maji
Ameyasema hayo kwenye ziara na Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi na Ofisi yake wakati walipotembelea Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira ya Chaani Kikobweni, kukaguwa majiko banifu kwa baadhi ya wananchi wa kijiji cha Matemwe
Majiko Banifu ya wananchi wa Kijiji cha Matamwe yanatokana na Mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia ekolojia ambao umefadhiliwa na mfuko wa mazingira wa kimataifa (GEF) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Mhe Harusi amewapongeza wanajumuiya hao na kuwasisitiza kutovunjika moyo kwa juhudi wanazozichukuwa kutokana na baadhi ya watu wachache wanaowavunja moyo kwa kuikata miti bali wajitahidi kuwapa elimu na kutoa taarifa inapotokea uharibifu kwa vyombo vya sheria pamoja na Ofisi za Mkoa husika
Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak amewashauri wanajumuiya hao kuhakikisha wanapanda miti ya asili hasa ile ambayo awali ilikuwepo na sasa imeanza kupotea kuanza kuihuwisha ili hata vyanzo vya maji ikiwemo mito na chemchem kuhuwika vyema.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Mhe Machano Othman Said ameushauri uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kukaa pamoja na kushirikiana na Wizara ya Kilimo Umwagiliaji mali asili na mifugo Zanzibar ili kukubaliana aina za miti inayopaswa kupandwa ambayo haiathiri mazingira
Mhe Machano ametoa wito kuwa zinapotokea siku za kitaifa hasa siku ya mazingira kuhakikisha wanajumuiya hao katika eneo lao wanakuwa na shughuli yeyote ya kimazingira kwa kupanda miti inayoendana na hali halisi ya eneo husika pamoja na kuwapatia elimu kuhusiana na uhifadhi hasa pembezoni mwa vyanzo vya maji
Katika risala yao ilisomwa na Bi Mwanaisha Makame Abdalla kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuiya hio Bw Msikitu Juma Haji waishukuru Idara ya Mazingira kwa mashirikiano wanayoyapata ikiwemo kuwapatia elimu, vitendea kazi na kukuza mashirikiano na Jumuiya nyengine
Hata hivyo wamesema changamoto kubwa waliyonayo ni uvamizi wa watu wasiojulikana kukata miti mikubwa katika maeneo yao ya uhifadhi, kulima karibu na mito, kuingiza wanyama kwenye vianzio vya maji na kusababisha uharibu wa vianzio vya maji
Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi imeridhishwa na maendeleo ya Miradi ya Uviko 19 na miradi ya Maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na ile yawananchi inayoanzishwa na kusimamiwa na Idara ya Mazingira
Ziara hio imeongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak, wajumbe wa Kamati, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Bw Sheha Mjaja, Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bi Farhat Mbarouk na watendaji wa Ofisi hio wengine Katibu tawala Mkoa wa Kaskazini Unguja Bw Makame Machano Haji, Mbunge wa Jimbo la Chaani Mhe Juma Usonge na baadhi ya watendaji wa Ofisi hio.