Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Harusi Said Suleiman amesema kwa juhudi kubwa za kupambana na Dawa za Kulevya Nchini,Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imepania kwa hamu kubwa kuwakamata waanzilishi na waingizaji wakubwa wa Dawa za Kulevya(MAPAPA).
Ameyasema hayo leo Februari 29,2024 kwenye Baraza la 10 la Wawakilishi wakati akijibu ombi la Muakilishi kupitia Viti Maalumu Visiwani Pemba Mhe.Shadia Mohamed Suleiman ,aliyependekeza kukamatwa zaidi kwa waauzaji na waingizaji wakubwa(MAPAPA) badala ya wasambasaji wadogo.
“Ni kweli kwa juhudi kubwa tunakamata,lakini tunaowakamata ni wale watumwa(wadogo) wanaopewa wakauze ila tunahamu ya kuwakamata Mapapa(wakubwa)” Alisema Waziri Harusi.
Aidha ,Mhe.Harusi amewataka waheshimiwa wenzake na wananchi kutoa taarifa kamili za vigogo wanaohusika kuingiza Dawa za Kulevya nchini na kuahidi zawadi maalumu kwa mwananchi yoyote atakaetoa taarifa kamili za kuwakamata mapapa.