Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akishiriki akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Ugawaji wa Vifaa Visaidizi kwa Watu Wenye Ulemavu, huko Ukumbi wa Sheikh Idris AbduKikwajuni, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja; Aprili 23, 2025.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka nchi ya Qadar imetoa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu zaidi ya mia tatu Zanzibar ambavyo vimegharimu Shilingi za Kitanzania Milioni 318.
Hafla hiyo ya ugawaji wa vifaa saidizi hivyo imefanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil (Baraza la Wawakilishi la Zamani) Kikwajuni, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja; Aprili 23, 2025.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali itaendelea kushiriana na wadau wa maendeleo wa Ndani na Nje ya Nchi, katika kuhakikisha Jamii ya Watu wenye Ulemavu, wanapata misaada na huduma stahiki za kuendelea.
Amesema kuwa ipo haja kwa Jamii kuchukua tahadhari ili kuepusha wimbi la watu wenye ulemavu hapa, hali ambayo inashuhudiwa sasa siku hadi siku, ambapo Zanzibar imeshuhudia Ongezeko kubwa, kiwango ambacho siyo cha kuridhisha hata kidogo.
Ameeleza kwamba kwamujibu wa Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2022, ongezeko la Idadi ya Watu wenye Ulemavu, kwa Zanzibar, ni kutoka Asilimia 5.8 hadi Asilimia 10.4.
Ametaja sababu za ajali barabarani, maradhi yasiyo ya kuambukiza, hasa yale yanayotokana na utaratibu usiofaa wa matumizi ya vyakula.
"Hivyo kwa niaba ya Serikali niseme tutaimarisha pia barabara zetu, na tutaweza kupunguza pia idadi ya Watu wenye Ulemavu", ameeleza Mheshimiwa Othman akiendelea kuorodhesha sababu zinazochangia ongezeko hilo.
Akitathmini hali ya Ongezeko la Watu wenye Ulemavu kwa sababu za kisiasa Mheshimiwa Othman amesema, "tumeshuhudia hapa Uchaguzi Mkuu uliopita uliwapa Watu Ishirini na sita (26) Ulemavu wa Kudumu; watu hawakuwa wanasiasa wala wana- hamasa, bali ni raia waliokuwa wanaendelea na shughuli zao; kwa hivyo nitoe wito kwa sote tunahusika, ni wajibu wetu kuhakikisha tunalipitisha zoezi hili kwa haki na salama".
Aidha amewahimiza Taasisi ya 'Qatar Charity' kuanzisha Ofisi yake hapa Visiwani Zanzibar, ili kuwa karibu katika kuratib na kutoa misaada ya kibinaadamu, na kwa ufanisi zaidi.
Akitoa Salamu za Wizara, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Harous Said Suleiman, ametoa wito kwa Wafadhili wa Ndani na Nje ya Nchi, kujitokeza na kuzidi kuunga-mkono juhudi za Serikali, katika kuimarisha Ustawi wa Jamii, na hasa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu.
Naye, Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Misaada ya Kibinaadamu, ya Nchini Qatar (Qatar Charity), Bw. Amjad Al-tahan, ameahidi kuendeleza mashirikiano na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, katika kusaidia Watu wenye Ulemavu, ili kuendeleza juhudi za kujenga ustawi bora kwa makundi yote.
"Kwetu sisi tunajisikia faraja kuwa sehemu ya kusaidia kundi hili la watu wenye ulemavu", ameeleza.
Ugawaji huo wa Vifaa Visaidizi umehusisha vitu mbali mbali kwaajili ya Watu wenye Ulemavu vikiwemo Viti-Mwendo vya Kawaida na vya Moto, Vyerehani, Mashine za Kupimia Shinikizo la Damu, na Fimbo kwaajili ya Wenye Ulemavu wa Macho.
Hafla hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kupitia Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, chini ya ufadhili wa Taasisi ya Misaada ya Kibinaadamu Nchini Qatar (Qatar Charity).