Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar

📢

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

Hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa CADiR
madiinat al-bah
January 1, 1970
Project Image
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema Serikali itaendeleza juhudi na kutoa mashirikiano ya kutosha, kuunga-mkono Miradi ya Watu Wenye Ulemavu, ili kuhakikisha Taifa linakuwa na Jamii Jumuishi. Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika Hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa CADiR (Collective Action for Disability Rights), huko katika Hoteli ya Madiinat Al-Bahr, Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Amesema Serikali, kama ilivyo kwa kila Mamlaka husika, inapaswa kuchukulia kwamba, Suala la Haki na Fursa kwa Watu Wenye Ulemavu ni Jambo la Wajibu kwa Nchi; linakuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida, na linalohitaji mashirikiano, ili kujenga Jamii Bora yenye Ustawi. Mheshimiwa Othman, ameainisha juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali, katika kujenga Ustawi wa Watu Wenye Ulemavu Nchini, zikiwemo za Kufanikisha uwepo wa Sheria na Sera Maalum za Kuilinda Sehemu hiyo Muhimu ya Jamii; Uimarishaji wa Miundombinu Rafiki; na Mifuko ya Fedha kwaajili ya Watu Wenye Ulemavu. Ameongeza kwa kusema, "licha ya juhudi hizo na nyengine mbali mbali zinazotekelezwa na Serikali, kwa kuimarisha Ustawi wa Watu Wenye Ulemavu Nchini, bado mahitaji yao ni mengi, ambapo imani yetu ni kwamba, kupitia Mradi huu, tutaongeza uwezo wa kulifikia Kundi hilo, na kuhamasisha upatikanaji wa haki na fursa, kwaajili ya maendeleo yao". Akifafanua juu ya malalamiko dhidi ya tabia isiyofaa, ya kuwatumia vibaya Watu Wenye Ulemavu, ikiwemo kuwaweka Barabarani kuomba pesa, Mheshimiwa Othman ametoa maelekezo akisema, "tatizo letu ni 'kuangaliana usoni, siyo kuangaliana mabegani', kila jambo kwetu ni siasa; naamini wahusika wanajulikana walipo, wanapohifadhiwa, tangu wanapowasili, wanakotokea na wanakokwenda; wanajulikana, wale 'Mapapa pamoja na Wadogo-Wadogo', na kwa hili naomba tusilichukulie kisiasa". "Nataka kusema kwamba Sheria na Sera Nzuri zipo, na zimeeleza wazi wazi juu ya kuwalinda Watu Wenye Ulemavu; pamoja na Mikataba ya Kimataifa, bali katika utekelezaji sijui tunakwama wapi", amefahamisha na kuhoji. Akihusisha Suala la Amani ya Nchi na Ulemavu, Mheshimiwa Othman amesema, "napenda nizidi kuwakumbusha kuwa, Mienendo yetu ya Maisha, Majukumu yetu, Amri zetu tunazotoa na tunazopokea , pamoja na azma zetu zote, katu zisitupelekee kuweka rehani uhai na uzima wa Watu wa Nchi yetu; tuepuke kwa kadiri ya uwezo wetu, kuongeza kwa makusudi, idadi ya Watu Wenye Ulemavu, na hilo linawezekana, iwapo tutaheshimu na kulinda haki, siyo tu za binaadamu, bali hata za kila kiumbe". Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman, ameutaja Mradi huo kwamba ni faraja kubwa, na ni sehemu ya kuungamkono Juhudi za Serikali, katika kujenga ustawi wa Watu Wenye Ulemavu, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amepongeza juhudi za Viongozi wakuu kwa kile alichosema kuweka mazingira yanayotoa haki na fursa kwa Watu Wenye Ulemavu. Katika Salamu zake, Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameeleza matumaini ya Serikali, kupitia Wizara yake, katika utekelezaji wa Mradi huo, ambao ni faraja kwa Watu wote. Ameinasihi Jamii kutosita kupata Ushauri kutoka kwa Wataalamu wa Afya, ili kuhakikisha Usalama wa Vizazi, na ikibidi kupunguza idadi ya Watoto Wanaozaliwa na Ulemavu. "Pamoja na kwamba Watu Wenye Ulemavu, katika Wizara ya Afya tunawapa 'first priority' (kipaumbele) katika huduma zetu, bali nawaomba Wananchi wote, Madereva wa Boda Boda na kila mmoja, tuepushe ajali, tujitahidi kulinda usalama wa watu wetu ili tuweze kupunguza idadi ya Watu Wenye Ulemavu", amesema. Kwa upande wake, Mshauri Mkuu kutoka NAD (Norwegian Association for the Disabled), Bi Elise Bjastard, amepongeza kasi ya Serikali zote Mbili, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT), na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), katika kuhamasisha Maendeleo na Ustawi wa Watu Wenye Ulemavu, hatua ambayo imepelekea Nchi yake ya Norway, kuridhia utekelezaji wa Mradi huo. Amehimiza Mashirikiano ya Wadau wote wa Mradi huo akisema, "tukishikamana pamoja tunaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi". Uzinduzi huo umeshuhudia Harakati mbali mbali zikiwemo za Wimbo Maalum wa Watoto Wenye Ulemavu; na Burdani ya Ngoma ya Kibati kutoka Kikundi cha Sanaa cha Taifa Zanzibar. CADiR ni Mradi wa Miaka Mitano (5) wa Kukuza na Kuimarisha Haki za Watu Wenye Ulemavu, Zanzibar na Tanzania Bara, unaoanza utekelezaji wake Mwaka huu wa 2025, na ambao umefadhiliwa na Serikali ya Norway, kupitia NAD. Viongozi mbali mbali wa Serikali, Watendaji na Wakuu wa Taasisi za Kitaifa na Kimataifa, Wanadiplomasia, Asasi za Kiraia, Vikosi vya Ulinzi na Usalama,Watu Wenye Ulemavu, Walimu na Wanafunzi, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Unguja, Ndugu Amour Mmanga, wamehudhuria katika Hafla hiyo.
Scroll to Top