Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Harusi Said Suleiman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupambana na waingizaji na wasambazaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kulinda ustawi wa wananchi na nguvu kazi ya Taifa.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Matumizi na Usambazaji wa Dawa za Kulevya yaliyofanyika katika hospitali ya Kidongo Chekundu, Wilaya ya Mjini, Mhe. Harusi amesema serikali haitawavumilia watu wanaohatarisha mustakabali wa taifa kwa kuendeleza biashara hiyo haramu.
“Serikali haitawafumbia macho watu wanaoingiza na kusambaza dawa hizi zenye kuathiri nguvu kazi ya taifa letu, hususan vijana walio katika umri wa chini ya miaka 18 ambao ndio waathirika wakuu wa janga hili,” alisema Mhe. Harusi.
Aidha, aliwataka wananchi wote kushirikiana na vyombo vya dola kwa kuwafichua wanaojihusisha na biashara hiyo haramu, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja katika jamii.
“Wazazi na walezi, chukueni jukumu la kuwaelimisha watoto wenu juu ya athari za matumizi ya dawa hizi ili kuwakinga na mtego wa kuharibikiwa maisha,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kinga, Tiba na Marekebisho ya Tabia, Bw. Juma Abdul-rahman Zidikheiry, ambaye alizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, alieleza kuwa waraibu wa dawa hizo wanapaswa kupewa nafasi ya pili katika jamii na kusaidiwa kupona, badala ya kunyanyapaliwa.
Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Bi. Maryam Juma Abdalla, alisisitiza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameendelea kuwa kinara na mfano wa kuigwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ambapo juhudi zake zimeleta mabadiliko chanya katika udhibiti wa matumizi ya dawa hizo.
Kwa upande wa waraibu wa zamani, Rajab Haji Abdalla kutoka Mangapwani alielezea shukrani zake kwa serikali kwa kuanzisha hospitali ya matibabu ya uraibu wa dawa za kulevya, akieleza kuwa tangu aachane na matumizi hayo amekuwa salama kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.
“Tunaomba vijana wenzangu wanaoendelea kutumia dawa hizi wajitokeze kupata msaada, kwani hakuna lisilowezekana tukijitambua na kupata msaada sahihi,” alisema.
Siku ya Kupambana na Matumizi na Usambazaji wa Dawa za Kulevya huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Juni, ikiwa ni kumbukumbu ya juhudi za kimataifa na kitaifa za kukabiliana na athari za dawa hizo kwa jamii.