OMKR NA ZEEA ZASAINI HATI YA UTOAJI WA MIKOPO WA 442 KWA MTU MMOJA MMOJA MWENYE ULEMAVU.
zeea
November 7, 2025
Katika Kutatua changamoto za watu wenye Ulemavu juu ya upatikanaji wa mikopo inayotolewa na Serikali, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu imetiliana saini ya hati ya makubaliano na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar ( ZEEA) juu ya utoaji wa mikopo wa 442 kwa mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu ili kuhakikisha watu hao wanapata fursa bila ya vikwazo, hafla ya utiaji saini imeanyika katika ukumbi wa mikutano wa ZEEA - Mwanakwerekwe, Unguja: tarehe 11 Julai,2025.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Harusi Said Suleiman amesema makubaliano hayo ni muhimu katika kuondosha changamoto zilizokuwa zikiwapata watu wenye Ulemavu za kupata mikopo ambazo ziliwafanya kupoteza matumaini ya kujiendesha kiuchumi pamoja na kujikwamua na umasikini.
Alisema ni imani kwamba kitendo hicho kitaamsha ari zao kufikia malengo yao ya kujiletea maendeleo kupitia mikopo hiyo na kujisikia miongoni mwa jamii kwani Serikali yao inawajali.
Hatahivyo, Waziri Harusi alibainisha kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ina mpango maalumu wa kuhakikisha wanakasimu na kuweka kiasi cha fedha ili mpango wa kuwapatia mikopo watu hao linaendelea.
Alisema wameona ni vyema mkopo wa watu wenye ulemavu uendane na mtu mmoja mmoja kuliko kwenye kundi hivyo amewataka watu hao kuhakikisha mikopo wanayochukua wanakwenda kuifanyia kazi kama ilivyokusudiwa na kuirejesha ili na wengine waweze kupata.
Kwa upande, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Mhandisi Ussi Khamis Debe amesema kundi hilo lilikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutoifikia mikopo kutokana na miongozo iliyopo ndani ya vikundi na aina ya ulemavu ya watu hao kushindwa kujumuika kwenye vikundi kupata mikopo, hivyo kupitia hati za muongozo huu utamuwezesha mtu mwenye ulemavu kupata mikopo bila ya kuhitaji kutoka kwenye kundi.
Pia, Mhandisi Debe ameipongeza Serikali kupitia Wizara hiyo kwa maslahi ya watu ambao hawana sauti kuwasemea na kufanya maamuzi hayo na mkataba huo utakuwa ni kufungua fursa kwa kundi hilo na anaamini wengi watanufaika kupitia watu wenye ulemavu ambao ni 160,000 sawa na asilimia 10 ya watu wote wanaoishi Zanzibar.
“ Serikali imetenga shilingi milioni 560 kwa ajili ya watu wenye ulemavu lakini mpaka sasa ni milioni 66 tu zimechukuliwa na kiwango kikubwa cha fedha kimebaki.
Hadi kufikia Juni 30 mwaka huu ZEEA imetoa shilingi bilioni 41.2 na kuwafikia wanufaika 24,478 na katika makusanyo waliopata ya shilingi 3.2 kutoka Halmashauri zote za Unguja na Pemba, ikiwa tayari imeshatoa bilioni 1.7 ambazo asilimia 26 vijana na asilimia 6 imewafikia watu wenye ulemavu “ Takwimu kutoka ZEEA.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia sekta ya watu wenye ulemavu(Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu) inazitakata jumuiya na vikundi vya watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kwa watu wenye mahitaji maalumu ili kuwanufaisha kiuchumi.
Kulingana na changamoto wanazopitia watu wenye ulemavu katika ukopeshwaji wa mikopo yenye malimbikizi ya riba ambao imekuwa ni kikwazo katika kujikwamua kiuchumi na inayokamisha malengo yao.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar ( ZEEA) na Baraza la taifa la watu wenye ulemavu imeanzisha mikopo nafuu isiyo na riba kwa watu wenye ulemavu, miongoni mwa mikopo hiyo ikiwemo huu wa “four four two” ambao unawasaidia na kuwawezesha kujikwamua kimaisha na kuondoa dhana ya utegemezi iliyozoeleka katika jamii.
Mikopo ya “four four two” ni mkusanyiko wa asilimia kumi(10) maalumu za pesa ambazo zinakusanywa katika kila halimashauri ya Unguja na Pemba, na kuwasilishwa katika mamlaka ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi(ZEEA).
“Four Four Two” hili neno linatokana na uwepo wa mgawanyo wa asilimia 10 za mikopo;
Mgawanyo wa asilimia “four” ya kwanza ni ya vijana wote( Wenye ulemavu na wasio na ulemavu),
na “four” ya pili ni kwa wanawake( wenye ulemavu na wasio na ulemavu yaani watuwazima,wenye umri wa kati au umri mdogo kuanzia miaka 18 )
na “two” ni asilimia za watu wenye ulemavu pekee.
Katika utoaji wa mikopo ya “four four two” imejigawa katika makundi matatu; kundi la kwanza ni mkopo mkubwa, la pili ni katinakati na la tatu ni mkopo mdogo, kulingana na uwepo wa makundi haya watu wenye ulemavu wanauwezo wa kuchukuwa mkopo katika kundi lolote kati ya hayo kulingana na masharti na vigezo vya uombaji.
Halikadhalika kupitia utiaji wa hati mpya ya leo utawawezesha mtu wenye ulemavu mmoja mmoja kupata fursa na kunufaika na mkopo huu wa 442.