Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi wa nyumba za wafanyakazi wa hospitali ya wilaya ya Wete, huko Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Pemba;tarehe 24 Disemba 2024 ikiwa ni sehemu ya Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka '61' ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kusimamia na kuhakikisha watoa huduma za afya wanapatiwa maakazi mazuri ili kutoa huduma bora kwa wananchi, na kuwaongezea ufanisi zaidi, katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo,Jumanne Disemba 24, 2024 akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi wa nyumba za wafanyakazi wa hospitali ya wilaya ya Wete, huko Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema ujenzi wa makaazi ya wafanyakazi, karibu na hospitali au jirani na vituo vyao vya kazi, lengo lake ni kuwapunguzia masafa pamoja na gharama za usafiri kwa kuwafata madaktari bingwa, na ili kuimarisha huduma za matibabu na kuhakikisha kila muhitaji anapata matibabu kwa wakati.
“Nyumba hizi zinazojengwa na zinatarajiwa kuhudumia makaazi ya takriban Familia 16, zitakua msaada mkubwa wa kurahisisha kazi za wafanyakazi. Hivyo ni vyema kuzingatia kuwa wakati mtakapo-zitumia, muzitunze ipasavyo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu, na ili kutimiza lile lengo lililokusudiwa” amesisitiza Mheshimiwa Othman huku akiwataka Wizara ya Afya kufikiria namna bora ya kuzitunza, ikibidi kabla ya kukamilika ujenzi; kwa kuweka utaratibu mzuri wa matunzo, ikiwemo kuzifanyia ukarabati kwa wakati stahiki.
Aidha amewaagiza Waziri wa Afya Zanzibar na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, kutumia jitihada za pamoja ili kuweka sawa miundombinu ya barabara kutoka njia kuu ya kinyasini mpaka ilipo hospitali hio, ili kuwapa wepesi wananchi kuifikia, hususan mama wajawazito na wasiojiweza, pamoja na kuwataka wananchi kuendelea kutoa mashirikiano ya dhati, kwa kutumia Hospitali hiyo ipasavyo kupata matibabu na kufanya uchunguzi wa afya kwa kufuata taratibu za rufaa kama miongozo ya Wizara ya Afya inavyoelekeza.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, amesema "Hospitali hizi za Wilaya zitakuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa mbali mbali ikiwemo huduma ya uzazi ambayo ilikuwa ni changamoto ya mda mrefu" ameeleza Mazrui huku akiwataka wafanyakazi wa sekta ya afya kuwajibika na kujitahidi kuhudumia wananchi.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Ndugu Salama Mbarouk Khatib, amesema takriban miradi 16 inayotarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na ufunguzi katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ni fursa kubwa ya kuchagiza maendeleo katika Mkoa huo.
Akiwasilisha taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dokta Mngereza Mzee Miraji, amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni nne nukta moja(4.1), itakuwa ni fursa adhimu ya kukuza sekta ya Afya kisiwani Pemba.
Aidha,hafla hiyo ilikuwa ni sehemu ya Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka '61' ya Mapinduzi ya Zanzibar, yanayobeba kaulimbiu ya 'Amani, Umoja na Mshikamano kwa maendeleo yetu.